Rais wa Marekani Donald Trump leo anawaleta pamoja viongozi wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, kwa kile atakachojipigia kifua kuwa ni hatua yake ya karibuni ya kusitisha vita.
Rais Paul Kagame ambaye ameiongoza Rwanda kwa muda mrefu, atakutana na Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, huku Trump akiwa na matumaini kuwa kutiwa saini kwa mkataba huo wa usitishwaji vita, utafungua njia ya Marekani kuchukua udhibiti wa madini muhimu mashariki mwa Kongo, eneo lililozongwa na mapigano ambalo pia lina utajiri mkubwa wa madini yanayotumika kwa teknolojia za kisasa.
Ikulu ya White House imesema kuwa Kagame na Tshisekedi watasaini mkataba wa amani, miezi mitano baada ya mawaziri wao wa mambo ya kigeni kukutana na Trump na kutangaza mkataba mwengine wa kusitisha vita.
Hatua ya kutiwa saini mkataba huo kati ya Kagame na Tshisekedi huko Marekani, kumeshuhudiwa mapigano makali huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, ambako waasi wa M23 katika wiki za hivi karibuni, wamekuwa wakisonga mbele na kulizidi nguvu jeshi la Kongo.
Chanzo; Bongo 5