Rais wa Marekani Donald Trump ametia saini amri ya kiutendaji itakayoongeza upatikanaji wa bangi, hatua iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu na inayotajwa kuwa mabadiliko makubwa zaidi ya sera ya dawa za kulevya nchini Marekani katika miongo kadhaa.
Kupitia amri hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Marekani ameagizwa kuainisha upya bangi kutoka Ratiba ya Kwanza (Schedule I) kwenda Ratiba ya Tatu (Schedule III), hatua inayoiweka bangi katika kundi moja na dawa kama Tylenol yenye codeine.
Hata hivyo, bangi itaendelea kuwa haramu katika ngazi ya serikali ya shirikisho. Pamoja na hilo, kuainishwa kama dawa ya Ratiba ya Tatu kutaruhusu tafiti zaidi kufanyika kuhusu manufaa yake ya kiafya.
Baadhi ya wabunge wa chama cha Republican wameonya dhidi ya hatua hiyo, wakidai kuwa inaweza kuhalalisha au kuzoesha matumizi ya bangi katika jamii.
Kwa mujibu wa Shirika la Kudhibiti Dawa za Kulevya la Marekani (DEA), dawa zilizo katika Ratiba ya Tatu—ikiwemo ketamine na anabolic steroids—zina “uwezekano wa kati hadi mdogo wa utegemezi wa kimwili na kisaikolojia.”
Akizungumza Ikulu wakati wa hafla ya kutia saini amri hiyo Alhamisi, Trump alisema watu wengi wamekuwa wakimsihi afanye mabadiliko hayo, hususan wale wanaokabiliwa na maumivu makali, ikiwemo wagonjwa wa saratani, wenye matatizo ya degedege, maumivu yasiyotibika, pamoja na maveterani wenye majeraha yaliyotokana na utumishi wao.
Rais huyo alifananisha bangi na dawa za kutuliza maumivu zinazotolewa kwa maagizo ya daktari, akisema zina matumizi halali lakini pia zinaweza kusababisha madhara makubwa yasiyorekebishika endapo zitatumiwa vibaya.
Uainishaji mpya pia una athari za kikodi kwa maduka ya bangi yaliyoidhinishwa na majimbo, kwani kwa sasa sheria zinayazuia kupata baadhi ya misamaha ya kodi endapo yanauza bidhaa zilizo katika Ratiba ya Kwanza.
Mbali na kuainisha upya bangi, Trump pia amewaagiza maofisa wa Ikulu kushirikiana na Bunge ili kuruhusu baadhi ya Wamarekani kupata cannabidiol (CBD).
Chanzo; Bongo 5