Mamlaka nchini Benin imetangaza kufanikiwa kuzima jaribio la mapinduzi lililolenga kumuondoa madarakani Rais Patrice Talon ambaye baadaye alilihutubia taifa na kuthibitisha kuwa hali imedhibitiwa kikamilifu na kwamba usaliti huo utaadhibiwa.
Kundi la wanajeshi kadhaa walitangaza hapo jana kwenye televisheni ya taifa kuipindua serikali na kuifunga mipaka yote ya nchi hiyo na kumteua Luteni Kanali Pascal Tigri kuwa rais wa kile walichokiita " tume ya mageuzi ya kijeshi." Baadaye wanajeshi kumi na wawili walikamatwa wakiwemo waliohusika na tukio hilo.
Umoja wa Afrika umelaani jaribio hilo la mapinduzi huku Jumuiya ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS ikitangaza kutuo msaada wa kijeshi kwa kutuma kikosi maalum nchini humo ili kuiunga mkono serikali na jeshi la Benin kwa lengo la kudumisha utaratibu wa kikatiba.
Jaribio hilo la mapinduzi limeshuhudiwa wakati Rais Patrice Talon, aliye madarakani tangu mwaka 2016, anatarajiwa kumaliza muhula wake wa pili na wa mwisho mwaka ujao wa 2026, na uchaguzi wa rais ukitarajiwa kufanyika Aprili mwakani.
Chanzo; Dw