Waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda wamedaiwa kutwaa mji wa Uvira ulioko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), na kuhatarisha makubaliano ya amani yaliyosainiwa hivi karibuni chini ya usimamizi wa Washington.
Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika, waasi hao waliingia viunga vya Mji wa Uvira jana, na kusababisha wakazi takribani 3,000 kukimbilia nchi jirani ya Burundi, huku vurugu hizo zukiibuka siku chache baada ya kuidhinishwa kwa makubaliano ya Kinshasa-Kigali yenye lengo la kurejesha amani mashariki mwa DRC.
Mpango huo mpya wa M23 na washirika wake wa Rwanda unakuja karibu mwaka mmoja baada ya shambulio kubwa lililowawezesha kuteka miji miwili mikubwa Goma na Bukavu.
Hata hivyo, Disemba 4, mwaka huu Rais wa Kongo Félix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda, Paul Kagame, waliidhinisha makubaliano huko Washington yenye lengo la kukomesha mgogoro huo, ambao Rais wa Marekani Donald Trump aliusifu kama muujiza.
Makubaliano hayo yanajumuisha sehemu ya kiuchumi inayoahidi kuhakikisha usambazaji wa madini ya kimkakati kwa ajili ya sekta iliyoendelea ya Marekani. Eneo la Mashariki mwa Kongo, eneo linalopakana na Rwanda na lina utajiri wa maliasili na linakabiliwa na migogoro kwa takribani miaka 30.
Chanzo; Nipashe