Serikali ya Ghana imetuma wanajeshi 54 nchini Jamaica kusaidia jitihada za ujenzi upya kufuatia uharibifu mkubwa uliosababishwa na kimbunga Melissa kilichokumba nchi hiyo mwezi Oktoba.
Wanajeshi hao, wanaotoka katika Kikosi cha 14 cha Wahandisi wa Jeshi la Ghana, watashiriki katika ukarabati wa barabara, ujenzi wa makazi ya muda, pamoja na kurekebisha miundombinu muhimu ya umma iliyoharibiwa na kimbunga hicho.
Ujumbe huo ni sehemu ya dhamira ya Ghana ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kutoa msaada wa kibinadamu na kuonyesha mshikamano na mataifa ya Caribbean yanayoathiriwa na majanga ya asili. Hatua hiyo pia iliungwa mkono na serikali ya Marekani, ambayo ilitoa ndege ya kijeshi ya mizigo aina ya C-17 kuwasafirisha wanajeshi wa Ghana pamoja na vifaa vyao hadi Kingston, Jamaica.
Akizungumzia hatua hiyo, Rais wa Ghana, John Dramani Mahama, alisema taifa hilo linaelewa maumivu ya majanga ya asili na safari ndefu ya kupona, hivyo dhamira hiyo inaonesha kujitolea kwa Ghana katika kutoa msaada wa kibinadamu, kurejesha na kujenga upya maeneo yaliyoathiriwa, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa Kusini kwa Kusini, mshikamano wa Pan-Afrika na Afro-Caribbean.
Mbali na kupeleka wanajeshi, serikali ya Ghana tayari imetuma misaada ya kibinadamu ikiwemo mchele, blanketi, magodoro, ndoo za plastiki na dawa kwenda Jamaica, Cuba na Sudan.
Kimbunga Melissa, ambacho ni cha kiwango cha tano, kilikumba Jamaica mwezi Oktoba na kusababisha vifo vya takriban watu 32, huku maelfu ya wananchi wakihitaji msaada wa chakula na huduma za msingi. Jamaica ni miongoni mwa nchi zinazokumbwa mara kwa mara na vimbunga, ambavyo mara nyingi huharibu makazi, hospitali na miundombinu muhimu.
Chanzo; Global Publishers