Mgombea wa urais kupitia chama cha National Unity Platform (NUP), Bw. Robert Kyagulanyi Ssentamu, amekabiliana na hali yenye mvutano na ulinzi mkali jana Jumamosi Disemba 6, 2025 wakati akifanya mkutano wake wa kampeni katika Jiji la Gulu, Kaskazini mwa Uganda.
Bobi alizuiwa katika Barabara ya Gulu Airfield na vikosi vya usalama vya UPDF na Polisi na kulazimika kuruka kutoka kwenye gari lake na kutembea kwa miguu, akiwa ameongozana na kikundi kidogo cha wanachama wa chama na walinzi wake.
Hata hivyo, vurugu zilitokea njiani wakati wanajeshi wa UPDF wakidaiwa kuwashambulia baadhi ya walinzi wake, na kuwajeruhi kadhaa, akiwemo msaidizi wake wa karibu, Dan Magic.
Kulikuwa pia na matukio ya makundi yasiyojulikana kushambulia wakazi katika maeneo kadhaa na katika eneo la kampeni la Kyagulanyi, ambako waliharibu vifaa vya muziki na kupiga mawe magari kabla ya polisi kuingilia kati.
Licha ya mvutano huo, Kyagulanyi alifanikiwa kufika katika uwanja wake wa kampeni na kupokewa kwa shangwe na wafuasiwake ambao walikuwa na wasiwasi, na mara kwa mara wakikimbia kwa hofu kutokana na wingi wa vikosi vya usalama.
Katika hotuba yake, mwanamuziki aliyegeuka kuwa mwanasiasa aliilaumu vyombo vya usalama kwa kujaribu kukandamiza kampeni zake kwa kuziba barabara na kuwatisha wafuasi wake.
Chanzo; Eatv