Shirika la Afya Duniani (WHO) imesema licha ya mafanikio ya mapambano dhidi ya malaria, ugonjwa huo kwa mwaka 2024 umeua watu 610,000.
WHO imetoa taarifa hiyo jana Alhamisi Desemba 4, 2025 ikieleza kuwa Idadi kubwa ya vifo hivyo ilitokea Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na watoto wakiwa miongoni mwa waathiriwa wengi zaidi.
Idadi ya takwimu walioumwa nayo imepanda kutoka milioni 273 hadi makadirio ya milioni 282, kwa mujibu wa ripoti hiyo ya malaria ambayo hutolewa na WHO.
Shirika hilo limetaja kuongezeka kwa usugu wa dawa, mabadiliko ya tabianchi na upungufu wa ufadhili kuwa miongoni mwa sababu zinazoathiri hali hiyo.
Limeonya kuwa maendeleo yaliyopatikana mwanzoni mwa miaka ya 2000 yako hatarini kuporomoka. Ethiopia, Madagascar na Yemen zimetajwa kuwepo maambukizi zaidi.
Malaria husababishwa na parasiti linaloenezwa kupitia kuumwa na mbu.
Mapambano ya kitabibu dhidi ya ugonjwa huu yamekuwa yakibadilika kulingana na kupatikana kwa dawa mpya, ingawa parasiti huyo huendelea kupata uwezo wa kuzipinga.
Mwanzoni mwa karne hii, usugu dhidi ya dawa ya chloroquine ulikuwa umeenea na malaria iliua zaidi ya watu milioni 1.8 kwa mwaka.
Baadaye kulikuja kundi la dawa lijulikanalo kama artemisinini, ambalo limesaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya malaria duniani.
Chanzo; Mwananchi