Brooklyn Peltz Beckham, mtoto wa kwanza wa nyota wa zamani wa soka David Beckham na mbunifu wa mitindo Victoria Beckham, amevunja ukimya huku akitoa kauli nzito kuhusu mgawanyiko uliopo kwa muda mrefu katika familia yake.
Kufuatia na chapisho aliloweka kwenye mitandao yake ya kijamii Brooklyn amesema alikaa kimya kwa miaka mingi kwa lengo la kulinda faragha ya familia yake. Lakini ameamua kuvunja ukimya huo baada ya familia yake kuendelea kuipotosha jamii katika vyombo vya habari.
“Nimekuwa kimya kwa miaka mingi na nimejitahidi kwa kila njia kuweka masuala haya kuwa ya faragha. Kwa bahati mbaya, wazazi wangu na timu yao wameendelea kwenda kwenye vyombo vya habari, jambo lililoniacha sina budi ila kujisimamia mwenyewe.
“Hivi karibuni nimeona kwa macho yangu mwenyewe ni kwa kiwango gani wako tayari kuweka uongo mwingi kwenye vyombo vya habari, na ninaamini ipo siku ukweli utakuja kugundulika wote,”ameandika Brooklyn
Aidha aliendelea kwa kueleza kuwa hajaamua kuzungumza hivyo kwa nia ya kutaka suluhisho bali ameona ni bora kuvunja uhusiano mazima, hata hivyo amekanusha vikali madai ya kuwa mke wake mwigizaji Nicola Peltz Beckham ndio chanzo cha yeye kugombana na familia yake.
“Mke wangu hanithibiti wala yeye sio chanzo cha yote haya. Kwa mara ya kwanza maishani mwangu, tangu nijitenge na familia yangu, wasiwasi huo umeondoka. Ninaamka kila asubuhi nikiwa na shukrani kwa maisha niliyoyachagua, na nimepata amani na nafuu,” aliandika.
Chanzo; Mwananchi Scoop