Liverpool inatajwa kuwa ndio timu iliyochaguliwa na mshambuliaji wa Bournemouth na timu ya taifa ya Ghana, Antoine Semenyo licha ya klabu nyingine za Ligi Kuu England zikiwemo Tottenham, Arsenal na Manchester City kuonyesha nia ya kutaka kumsajili.
Semenyo amekuwa akiwindwa na vigogo wengi barani Ulaya tangu dirisha lililopita la usajili wa majira ya kiangazi kutokana na kiwango chake bora alichoonyesha akiwa na Bournemouth.
Mkataba wa sasa wa Semenyo na Bournemouth unatarajiwa kumalizika mwaka 2030. Tangu kuanza kwa msimu huu, mshambuliaji huyo amecheza mechi 16 za michuano yote na kufunga mabao matano.
Semenyo amekuwa akihitajika na Liverpool tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi na inaonekana staa huyu amevutiwa sana na mipango yao.
Liverpool inataka kuhakikisha inamsajili Januari mwakani ili akazibe pengo la Mohamed Salah ambaye atakuwa anaitumikia Misri katika michuano ya AFCON kwa wakati huo.
Chanzo; Mwanaspoti