Kocha wa Tinu ya taifa ya Argentina Lionel Scaloni amerudisha Kombe la Dunia katika hafla ya Droo ya Makundi inayoendelea nchini Marekani, ikiwa ni ishara ya kuhitimisha ubingwa wao wa mwaka 2022 na kuanzisha rasmi mchakato wa kuelekea fainali zijazo za Kombe la Dunia 2026.
Hafla hiyo, iliyohudhuriwa na viongozi wa soka wa kimataifa, wawakilishi wa timu shiriki na mashabiki kutoka pembe zote za dunia, imepambwa na tukio hilo muhimu linaloashiria kufunguliwa kwa ukurasa mpya wa mashindano ya kihistoria ya mwaka 2026.
Kombe la Dunia 2026, ambalo litafanyika kwa mara ya kwanza katika nchi tatu Marekani, Mexico na Canada linatarajiwa kuwa na mvuto wa kipekee kutokana na ongezeko la timu shiriki kutoka 32 hadi 48.
Mashindano hayo yatafanyika kuanzia Juni hadi Julai 2026, yakitarajiwa kuwa na ushindani mkali na burudani ya hali ya juu kwa mashabiki kote duniani.
Kwa kurejeshwa kwa kombe hilo, ujumbe uliodhihirika ni kwamba ubingwa huo sasa 'upo wazi kuwaniwa' na mataifa yote yatakayoshiriki, huku timu ya Argentina ikitarajia kutetea taji lake dhidi ya wapinzani watarajiwa wenye nguvu na ari mpya.
Mashabiki wamepokea tukio hilo kwa hamasa, huku maandalizi ya mashindano hayo yakionekana kuendelea kwa kasi katika miji mbalimbali mwenyeji.
Fainali za Kombe la Dunia 2026 zinatarajiwa kuvunja rekodi ya idadi ya watazamaji na kutoa historia mpya katika mchezo wa soka duniani.
Chanzo; Mwanaspoti