Klabu ya Yanga ya mkoani Dar es Salaam imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la shabiki wake kuruka uzio na kuingia kwenye eneo la kuchezea (pitch), ambapo shabiki huyo alionekana kufika hadi kwenye goli la timu ya Coastal Union na kuinama kama Ishara ya kutafuta, kuchukua ama kuweka kitu.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Wakati huo huo, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania inazikumbusha klabu zake kuendelea kusisitiza umuhimu wa mchezo wa kiungwana na tabia njema mchezoni kwa wachezaji, viongozi na mashabiki wake. Ukumbusho huu unakuja kufuatia mfululizo wa matukio ya wachezaji kufanya vitendo visivyo vya kiuanamichezo kwa wachezaji wenzao ikiwemo kupiga.
Pamoja na kuhatarisha usalama wa wachezaji, matukio hayo pia yamekuwa yakileta taswira mbaya kwa Ligi yetu jambo ambalo linaweza kushusha hadhi yake na kwamba licha ya adhabu kali ambazo zimekuwa zikitolewa kwa wachezaji husika, bado matukio hayo yameonekana kuendelea viwanjani.
Chanzo; Mwanaspoti