Ryan Wedding, mwanariadha wa zamani wa Olimpiki wa Canada katika mchezo wa snowboard aliyebadilika na kuwa mtuhumiwa wa kuwa kinara wa biashara ya kimataifa ya dawa za kulevya, amerejeshwa nchini Marekani baada ya kukamatwa jijini Mexico City Alhamisi usiku. Kuna pia video inayoonyesha wakati aliposhuka kutoka kwenye ndege, akiwa amezungukwa na maafisa wa shirikisho.
Wedding, ambaye alikuwa kwenye orodha ya FBI ya Watu Kumi Wanaosakwa Zaidi, alitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Ontario siku ya Ijumaa, takribani maili 40 nje ya jiji la Los Angeles.
Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 44 alikuwa amevaa kofia nyeusi ya baseball, fulana nyeusi ya juu (vest), shati la ndani la rangi ya kijivu na suruali ya jeans, huku mikono yake ikiwa imefungwa pingu mbele alipokuwa akitembea akishuka kutoka kwenye ndege na kuvuka eneo la uwanja wa ndege.
Akisisitiza uzito wa kukamatwa kwake, Wedding alisindikizwa na Mkurugenzi wa FBI, Kash Patel, ambaye alimuelezea kama “mfanyabiashara mkubwa zaidi wa dawa za kulevya katika nyakati za kisasa.”
Alisema: “Huyu ni El Chapo wa kizazi cha sasa. Ni Pablo Escobar wa kisasa, na alidhani angeweza kukwepa mkono wa sheria.”
Canzo; Bongo 5