Kikosi cha mwisho cha wachezaji 28 wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kitakachoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 kuanzia Desemba 21, mwaka huu kimewekwa hadharani.
Kaimu Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Miguel Gamondi amepunguza wachezaji 27 kutoka katika kikosi cha awali kilichokuwa na wachezaji 55.
Idadi kubwa ya wachezaji waliopunguzwa ni wale wanaocheza katika klabu zinazoshiriki katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Uamuzi wa kushtukiza katika uteuzi wa kikosi hicho cha mwisho unaweza kuwa ule wa kuachwa kwa kiungo wa Yanga, Mudathir Yahya.
Mshambuliaji wa Simba, Selemani Mwalimu, naye hatokuwemo katika fainali za AFCON 2025 kama ilivyo kwa nyota wa Yanga, Offen Chikola.
Licha ya kuonyesha kiwango bora katika mchezo dhidi ya Simba ambao aliibuka Mchezaji Bora wa mechi, mshambuliaji Nassor Saadun wa Azam sio miongoni mwa nyota ambao Gamondi amechagua kwenda nao Morocco.
Kazi nzuri iliyofanywa na nyota wa JKT Tanzania ya kupachika mabao matano yaliyomfanya awe kinara wa Ufungaji katika Ligi Kuu Tanzania Bara hadi sasa, hakijatosha kumshawishi Gamondi kumuingiza katika kikosi chake cha mwisho kwa ajili ya AFCON.

Nahodha Mbwana Samatta anayecheza Le Havre ya Ufaransa, ataongoza kundi la wachezaji watakaopeperusha bendera ya Tanzania huko Morocco huku jina la Saimon Msuva anayecheza Al Talaba ya Iraq nalo likiwa kundini.
Chanzo; Mwanaspoti