STAA wa Morocco, Brahim Diaz amevunja ukimya kuhusu penalti aliyopiga kwenye mchezo wa fainali ya Afcon 2025 baada ya madai kuwa aliikosa kwa makusudi.
Diaz, ametoa tamko kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuwa adui namba moja wa umma kufuatia uamuzi wake wa kupiga penalti ya hatari aina ya Panenka katika dakika za mwisho za fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Diaz amejitokeza hadharani na kuomba radhi kwa mashabiki wa Morocco baada ya penalti mbaya iliyogharimu timu yake katika fainali ya AFCON. Jaribio lake la Panenka liliokolewa kwa urahisi na kipa Edouard Mendy katika dakika za mwisho za muda wa kawaida, huku Senegal baadaye wakinyanyua taji.
Jaribio dhaifu la Diaz liliwafanya baadhi ya mashabiki kubashiri kuwa alikosa kwa makusudi kama ishara ya mshikamano na Senegal, kufuatia uamuzi wenye utata wa mwamuzi Jean Jacques Ndala wa kutoa penalti hiyo.
Hata hivyo, madai hayo yalikanushwa baada ya mechi na Diaz alitumia mitandao ya kijamii siku ya Jumatatu kuomba radhi, alipoandika: “Moyo wangu unauma.
Niliota kushinda taji hili kutokana na upendo wote mlionipa, kila ujumbe, kila ishara ya kuniunga mkono iliyonifanya nijisikie siko peke yangu. Nilipigana kwa kila kitu nilichokuwa nacho. Jana nilishindwa, na nachukua jukumu kamili na naomba msamaha kutoka ndani ya moyo wangu.
Itakuwa vigumu kupona, kwa sababu jeraha hili haliponi kirahisi, lakini nitajaribu.
“Sio kwa ajili yangu, bali kwa ajili ya wote waliamini kwangu na kwa wote walioumia pamoja nami. Nitaendelea kupigana hadi siku moja niweze kulipa upendo huu wote na kuwa chanzo cha fahari kwa watu wangu wa Morocco.”
Chanzo; Mwanaspoti