Kila mshambuliaji mchanga anayesisimua anapimwa kwa kiwango cha Lionel Messi.
Vijana wawili walio katika kiwango cha juu ni Lamine Yamal - ambaye tayari ni supastaa wa kimataifa - na sasa Estevao Willian wa Chelsea.
Yamal, kama gwiji wa Argentina Messi, alitoka katika katika akademi maarufu ya Barcelona ya La Masia.
Estevao alitawazwa jina 'Messinho' - iliyotafsiriwa kama 'Messi mdogo' - kupitia mchezo wake katika ligi kuu ya Brazil, na ameanza vyema tangu ajiunge na Chelsea baada ya Kombe la Dunia la Vilabu majira ya kiangazi.
Alihama baada ya siku yake ya kuzaliwa ya 18, baada ya kukubali mkataba wa mapema mwezi Mei 2024 ambapo alijiunga kutoka Palmeiras kwa £29m, na dau la uhamisho huo kupanda hadi £ 51m pamoja na nyongeza.
Kwa kadiri rekodi zinavyoonyesha, mchezo wa Jumanne wa Ligi ya Mabingwa kati ya Chelsea na Barcelona Uwanja wa Stamford Bridge ulikuwa wa kwanza kwa Yamal kukabiliana na Estevao katika mechi rasmi. Vijana hao wenye umri wa miaka 18 walizaliwa miezi mitatu tofauti mwaka 2007.
Kwa sasa wanachukuliwa kuwa vijana wawili wenye thamani kubwa katika soka la dunia - kulingana na CIES Football Observatory, Yamal ana thamani ya £307.4m, Estevao akiwa wa pili kwa thamani ya £103.8m.
Mmoja wa watu wachache wenye uwezo wa kuwalinganisha washambuliaji hao wawili ni beki wa Chelsea, Marc Cucurella.
Amecheza na wote wawili, akimkaba Estevao kwenye Kombe la Dunia la Klabu wakati wa mechi ya mwisho ya winga huyo kwa Palmeiras.
Na siku ya Jumanne Estevao Willian alimshinda, Lamine Yamal katika ushindi wa 3-0 nyumbani dhidi ya Barcelona kwenye Ligi ya Mabingwa.
Estevao, 18, alifunga bao la pili la kushangaza baada ya wachezaji wa Barcelona kupunguzwa hadi 10 kupitia kadi nyekundu aliyopatiwa nahodha Ronald Araujo kabla ya kipindi cha mapumziko.
Cucurella alisema: "Nadhani wote wawili ni wachezaji maalum sana. Wana vipaji vingi, mara kwa mara wanataka mpira, ili kukabiliana moja kwa moja na mabeki. Ni wachezaji ambao wanaweza kuamua hatma ya mechi.
"Tofauti sasa ni kwamba Lamine amecheza Ulaya misimu michache. Estevao akiendelea na hilo, nadhani anaweza kufikia kiwango cha Lamine. Wanapenda mchezo, wanapenda mpira."
Chanzo; Bbc