Aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Algeria, Madjid Bougherra, ametangaza rasmi kuachana na kikosi hicho siku nane kabla ya kuanza kwa michuano ya AFCON, kufuatia kuondolewa kwa Algeria kwenye FIFA Arab Cup.
Bougherra, ambaye mkataba wake ulikuwa ukifikia tamati mwezi Desemba mwaka huu (2025), amesema kuwa safari yake na timu ya taifa ya Algeria imefikia mwisho. Akizungumza baada ya matokeo hayo, kocha huyo alibainisha kuwa ametoa mchango wake wote kwa timu na sasa ni wakati wa uongozi mpya kuendeleza jukumu hilo.
Kocha huyo ataendelea kukumbukwa kwa mafanikio makubwa aliyoyapata akiwa na Algeria, hususan kuiongoza timu hiyo kutwaa ubingwa wa FIFA Arab Cup mwaka 2021, mafanikio yaliyomweka katika historia ya soka la taifa hilo.
Uamuzi wa Bougherra unakuja wakati nyeti kwa Algeria, ikijiandaa kushiriki AFCON, huku mashabiki na wadau wa soka wakisubiri kwa hamu kujua ni nani atakayechukua nafasi yake kuiongoza timu hiyo katika mashindano hayo makubwa ya Afrika.
Chanzo; Global Publishers