Klabu ya Simba imethibitisha kumsajili beki wa kati, Ismael Touré (28), kama mchezaji huru baada ya kuvunja mkataba wake na klabu ya FC Baniyas ya Falme za Kiarabu (UAE).
Touré, ambaye ana uzoefu mkubwa wa soka la kimataifa, anajiunga na Wekundu wa Msimbazi akitarajiwa kuimarisha safu ya ulinzi katika mashindano ya ndani na kimataifa.
Beki huyo anajulikana kwa nguvu, uwezo wa kusoma mchezo na uzoefu wake katika ligi mbalimbali.
Kabla ya kucheza FC Baniyas, Ismael Touré aliwahi kuitumikia Stellenbosch FC ya Afrika Kusini, ambapo alifanya kazi chini ya Kocha Steve Barker na kuonesha kiwango kizuri kilichompa nafasi ya kuendelea na safari yake ya soka kimataifa.
Usajili wa Touré ni sehemu ya mkakati wa Simba kuimarisha kikosi chake kwa lengo la kufanya vizuri zaidi katika Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa, hususan Ligi ya Mabingwa Afrika.
Chanzo; Mwanaspoti