Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye amemtunuku Kocha Mkuu wa timu ya taifa, Pape Thiaw pamoja na wachezaji wa ‘Simba wa Teranga’ kwa kuwapa hadhi ya ‘Commander of the National Order of the Lion’, heshima ya juu ya kitaifa inayotolewa kwa watu waliotoa mchango mkubwa kwa taifa lao.
Tuzo hiyo imetolewa usiku wa kuamkia leo Jumatano Januari 21, 2026 kufuatia mafanikio ya Senegal kutwaa ubingwa wa AFCON 2025, baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Morocco katika fainali ya mashindano hayo.
Akizungumza katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo, Rais Faye amesema ubingwa wa AFCON 2025 umeiletea Senegal heshima kubwa barani Afrika na duniani kwa ujumla, akibainisha kuwa mafanikio hayo yameimarisha mshikamano wa kitaifa.
Ameongeza kuwa kocha na wachezaji wamekuwa mabalozi wazuri wa nchi kupitia michezo, wakionesha nidhamu, mshikamano na uzalendo wa hali ya juu.
Mbali na heshima hiyo ya kitaifa, Rais Faye amewazawadia wachezaji kila mmoja kiasi cha Dola 135,000 za Marekani (Sh342 milioni) pamoja na kipande cha ardhi chenye ukubwa wa mita za mraba 1,500 katika eneo la Petite Côte, huku kila mtu mmoja wa benchi la ufundi na watumishi wa timu akipokea Dola 90,000 (Sh228 milioni) na kipande cha ardhi cha mita za mraba 1,000.
Chanzo; Mwanaspoti