Safari ya bondia wa Timu ya Taifa ya Tanzania, maarudu kama FARU WEUSI, Faru – Faki Issa Faki “Fighter”, imeishia katika hatua ya 16 bora ya Ubingwa wa Dunia baada ya kupoteza pambano lake kwa points dhidi ya Saken Bibbosinov wa Kazakhstan.
Faki mwenye umri wa miaka 22 alipambana kwa ushindani mkubwa dhidi ya Bibbosinov, bondia namba 7 kwa ubora duniani katika uzani wa kilo 54 Bantamweight. Bibbosinov anatokea Kazakhstan, moja ya mataifa makubwa na yenye kufanya vizuri sana katika mchezo wa ngumi duniani.
Licha ya kupoteza pambano hilo, Faki amepata heshima kubwa kwa kuvunja rekodi ya miaka 51 ya Tanzania kutoshinda pambano katika mashindano ya Ubingwa wa Dunia. Rekodi hiyo ilikuwa ikishikiliwa tangu mwaka 1974, pale Emmanuel Mlundwa alipomshinda Alfredo Pereira wa Puerto Rico kwa points katika mashindano yaliyofanyika Havana, Cuba.
Hata hivyo, Faki amepishana kwa bahati mbaya na begi la hela la Tsh milioni 25 ambalo hutolewa kwa wanaofuzu hatua ya robo fainali, huku akiacha alama ya historia na matumaini mapya kwa ngumi za Tanzania.
Faki (jezi ya blue) na Bibbosinov (jezi nyekundu) wakati wa kumtangaza mshindi wa pambano lao katika Uwanja wa Tennis Dubai.
Chanzo; Bongo 5