Rose amesema alitokea kumuamini mtu wa karibu yake lakini alifanyiwa njama za udanganyifu hali iliyomsababishia akamatwe uwanja wa ndege alipokuwa kwenye maandalizi ya kwenda Marekani.
Rose Muhando alieleza changamoto na maumivu aliyopitia wakati huo yalimfanya akatunga wimbo wake maarufu uitwao ‘Nibebe’.
“Mungu aliniinua nikaimba ‘Mteule Uwe Macho’ na ‘Nibebe’. Nibebe ndio wimbo ambao utaishi kwa sababu nilipitia machungu makubwa duniani. Shetani alikuja kunifitini, nikafanyiwa uovu mwingi mpaka polisi nikapelekwa na kufungwa,” alisema.
Rose Muhando, alisema matatizo yake yalianza baada ya meneja wake wa kwanza kufikishwa gerezani, akiachwa peke yake na waimbaji wa kwaya ndipo mtu mmoja akaja na kudai angemsaidia katika huduma, lakini baadaye aliamua kuachana naye na kujitenga peke yake ndipo akapata mwaliko wa kufanya tamasha nchini Marekani.
“Baadaye, mtu mmoja ambaye hakuwahi kuniambia alikuwa anataka kunisaidia, alikuja akaniambia kuwa anataka kuwa meneja wangu. Niliamua kumwamini. Lakini mambo yakawa tofauti, sikupenda hali hiyo, hivyo niliamua kujitenga.”
Chanzo; Mwananchi Scoop