Ni zaidi ya mwaka sasa tangu rapa Young Lunya alipotoa albamu yake, Mbuzi (2024) na tangu wakati huo amekuwa kimya bila kutoa kazi yake binafsi kwa ajili ya mashabiki wake wanaozimikia muziki wa Hip Hop.
Albamu hiyo ilitoka Juni 28, 2024 chini ya Sony Music Entertainment East Africa Limited, lebo iliyomsaini hapo Juni 2022 akiwa ni msanii wa kwanza wa Hip Hop Bongo kupata dili hilo kubwa la usimamizi na usambazaji wa muziki wake.
Msimamizi wa Masoko na Maendeleo ya Wasanii Afrika Mashariki chini ya Sony Music Entertainment, Seven Mosha alishawishika na uwezo wa Lunya baada ya kuchana katika mdundo wa wimbo wa Ommy Dimpoz, Kata (2020).
Ikumbukwe rapa huyo alipata usikivu wa wengi akiwa kundi la OMG ambalo alikuwa na wenzake wawili, Salmin Swaggz na Conboi, na wote walisainiwa na Switch Music Group (SMG) yake Quick Rocka kisha kuvuma na ngoma yao, Uongo na Umbea (2017).
Hata hivyo, awali Young Lunya alifanya muziki katika kituo cha Mkubwa na Wanawe kilichowatoa wakali kibao Bongo kama Aslay na Mbosso, ila baada ya muda akaendelea na harakati zake nyingine hadi alipokuja kutoka.
Mei 2019 alianza kutoa mfululizo ngoma zake za michano (freestyle session), mradi ambao ulipata mapokezi mazuri huku wasanii wengi wakimuomba kolabo, baadhi yao ni Joh Makini, Mimi Mars, Professor Jay, Rosa Ree, Harmonize n.k.
Wimbo wake, Mbuzi (2021) ulipokelewa vizuri na kumuwezesha kushinda tuzo mbili za muziki Tanzania (TMA) 2021 kama Wimbo Bora wa Hip Hop na Msanii Bora wa Hip Hop akiwabwaga Nay wa Mitego, Professor Jay, Rapcha na Darassa.
Chanzo; Mwananchi Scoop