Rapa kutokea Marekani, 50 Cent anajulikana kuwa si mtu wa kuogopa kuingilia mijadala yenye utata kwenye mitandao ya kijamii, lakini anasema kuna mijadala ya aina mbili ambayo amekuwa akijiepusha nayo.
50 Cent, mkali wa kibao cha Candy Shop (2005), ameitaja mijadala ya kidini na kisiasa kama mambo ambayo amekuwa akijizuia kujihusisha nayo katika mitandao maana anajua athari zake.
Akizungumza huko West Hollywood wakati wa uzinduzi wa Moses the Black, filamu ambayo yeye ni mmoja wa watayarishaji wake, alieleza kwanini filamu hiyo imejikita kwenye burudani badala ya masuala ya kidini.
“Kuna mambo mawili wanakuambia uyaepuke. Wanakuambia ukae mbali na dini na ukae mbali na siasa, kwa sababu haijalishi unaamini nini, kutakuwa na mtu anayepingana na wewe kwa hisia kali,” alisema.
Aliwataja baadhi ya wasanii wenzake kama Nicki Minaj na Ye (zamani Kanye West) kama mifano ya wasanii ambao wamekuwa wakizungumza waziwazi kuhusu dini na siasa ila baadaye wakajikuta katika wakati mgumu.
“Mimi najiepusha na mambo hayo. Hapo ndipo Kanye West alipoharibu mambo. Halafu Nicki Minaj naye akasema maneno fulani. Inaonekana kama ni wazimu, lakini huo ndio ukweli wenyewe,” alisema 50 Cent.
Chanzo; Mwananchi Scoop