Umezoea kusikia maneno haya “msanii ni kioo cha jamii.” Mbali na maana hiyo soma hapa mwanamuziki wa hip-hop nchini Claudia Lubao maarufu ‘Chemical’ anaeleza maana ya msanii.
“Neno msanii linaenda mbali zaidi ya kauli tuliyozoea kusikia ya “kioo cha jamii.”
Msanii ni sauti ya wasio na sauti, wale wanaonyamazishwa na hofu, ukandamizaji, kunyimwa haki, au kukosa fursa na majukwaa ya kusikika.
“Katika historia ya binadamu, wasanii wamekuwa waandishi wa nyakati (chronicler of history), wakitafsiri yaliyopita, kukabiliana na yanayoendelea sasa na kuonya au kuashiria yajayo.
“Kwa maana hiyo, msanii anakaribia nafasi ya nabii wa kijamii, si kwa kutabiri, bali kwa kusema ukweli unaoweza kuumiza, kuponya au kuamsha fikra.
“Kuwa msanii ni wito, si bahati au kipaji pekee, na wito hubeba wajibu! Unapokuwa msanii, unakuwa mtu wa umma (Public figure; yaani mtu ambaye sauti, matendo na msimamo wake vinaathiri watu wengi, hata wale wasiomjua binafsi.
“Hivyo basi, uhuru binafsi hupungua, lakini uwajibikaji wa kijamii huongezeka. Leo, wengi wetu tunazalisha burudani pekee nyimbo za mapenzi, za kukimbia uhalisia, au muziki usio na ufahamu wa kijamii (unconscious) tukijisemea, “Hiki ndicho mashabiki wanataka.”
“Lakini swali gumu ni hili kwa nini pale wafuatiliaji wa kazi zetu (mashabiki) wanapotuhitaji zaidi, tunageuka kuwa daraja la kuwahalalishia wanaowakandamiza?
“Hapo ndipo mtu wa umma (msanii) anapogeuka kuwa mtu mwenye ubinafsi. Public figure anasahau maana ya public.
“Mwisho (kwa leo): Majukwaa tuliyonayo leo, heshima tunayopata, maisha tunayoyaishi na hasa maumivu na hasira za watu walizonazo juu yetu katika nyakati hizi, yote yamejengwa juu ya mapenzi na imani ya watu.
“Waliotegemea kwamba tutasimama pamoja nao, si juu yao. Ni huzuni kuona bado hatujaitambua thamani yetu kama wasanii, au tumeichagua kuibadilisha kwa ajili ya kukubalika na wakandamizaji.
“Na kabla hujasema, “Mimi ni mkubwa kuliko shabiki,” tafadhali rejea nyuma. Kabla ya subscribers, kabla ya followers, kabla ya likes, views na blue ticks, that humble beginning.
Chanzo; Mwananchi Scoop