Mwanamuziki mkongwe wa Bongofelva, Ferooz Mrisho maarufu kama Ferooz amedai wasanii wengi wa kiume wanataka mapenzi ya kweli kutoka kwa wanawake.
Ferooz aliyewahi kutamba na nyimbo kali kama Mkiwa, Starehe, Kamanda, Bosi na nyinginezo ameliambia Mwananchi Scoop kuwa mastaa wengi wa kiume wamegundua kwamba mapenzi ya kweli hayapo upande mmoja tu kwa mabinti, bali hata wao wanaume wanatakiwa kuwa kwenye mapenzi.
Ingawa hakutaka kuingia kwa undani, mwanamuziki huyo alisema zamani wasanii wengi wa kiume walitumia fedha kuwarubuni mabinti, lakini sasa mambo yamebadilika kwani wasanii wengi wanaume wanataka mapenzi ya dhati kutoka mioyoni mwa wapenzi wao.
"Wasanii wengi wa kike wamekuwa wakitajwa kuwa na mahusiano na wanaume wenye pesa, ila mimi nasema kwa upande wa wasanii wa kiume wanawapenda wanawake kutoka moyoni," alisema Ferooz.
Pamoja na kauli ya mkongwe huyo kumekuwapo na hisia mbalimbali kuhusu mahusiano ya wasanii, ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakidai kwamba mara nyingi hutumia fedha na umaarufu kuwarubuni mabinti ili kujihusisha nao kimapenzi.
Chanzo; Mwananchi Scoop