Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Abdulazizi Chende maarufu Dogo Janja ameapishwa leo Desemba 4, 2025 kuwa Diwani wa Kata ya Ngarenaro, Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Hata hivyo Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam wamemchagua Diwani wa Mchikichini, Nurdin Juma maarufu Shetta, kuwa Meya wa jiji hilo.
Shetta ambaye ni msanii wa muziki wa Bongo Fleva, anakuwa meya wa Jiji hilo akichukua nafasi ya Meya Omary Kumbilamoto aliyehudumu kuanzia mwaka 2021 hadi 2025.
Katika uchaguzi huo wajumbe 51 waliopiga kura wamemchagua Shetta kwa kura 48 huku kura mbili zikiwa za hapana. Kwa upande wake John Mrema ambaye ni Naibu Meya amepata kura za ndiyo 49.
Ikumbukwe katika mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM kumpata mgombea wa Umeya wa Jiji la Dar es Salaam katika uchaguzi uliofanyika Ukumbi wa CCM Wilaya ya Ilala, Shetta aliibuka mshindi baada ya kupata kura 25, akimshinda Diwani wa Kata ya Segerea, Robert Manangwa, aliyepata kura 21.
Ikumbukwe wasanii hawa sio pekee waliopata nafasi ya kuwatumikia wananchi kwa mwaka huu kwani yupo Clayton Chipando 'Baba Levo' ambaye ni Mbunge wa Kigoma mjini, Hamis Mwinjuma 'Mwana FA' Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na wengineo.
Chanzo; Mwananchi Scoop