Imeelezwa kwamba uwepo wa miradi ya graphite Mahenge, Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro itafungua fursa mbalimbali za kiuchumi kuanzia ngazi ya kijiji mpaka taifa kutokana na uwekezaji mkubwa unaotarajiwa kuwekezwa katika maeneo yaliyothibitishwa na kampuni mbili za uwekezaji Faru Graphite na Duma Graphite kupitia kampuni ya TanzGraphite.
Hayo yalibainishwa Novemba 11, 2025 na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga Juma Kapilima wakati akielezea kuhusu fursa za kiuchumi na kijamii zitakazojitokeza kupitia uwekezaji mkubwa unaotarajia kufanyika katika miradi ya madini ya kinywe.
Kapilima alisema kuwa, mradi wa faru graphite unatarajia kuleta ajira 900 za moja kwa moja na ajira 4000 zisizo za moja kwa moja ambapo kupitia nafasi hizo kutafungua ajira nyingine ndogo ndogo kwa jamii ya Mahenge na viunga vyake.
Akielezea kuhusu ujenzi wa miundombinu ya nishati ya umeme, Kapilima alisema kuwa, kupitia mradi huo kuna mpango wa kuvuta umeme wa kilovoti 220 kutoka Ifakara hadi Mahenge ikiwa pamoja na ujenzi wa miundombinu ya barabara zitakazo unganisha eneo la mradi na vitongoji na vijiji ili kurahisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.
Kwa upande wake Afisa Uhusiano wa Faru Graphite Jacqueline Mushi alisema kuwa, utekelezaji wa Mpango wa Wajibu wa Kampuni (CSR) tayari umeanza mpaka sasa umejenga Ofisi za vijiji 3 ikiwa ni kijiji cha mdindo, kisewe na mdindo.
Pia mradi umechangia mifuko 100 ya simenti kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Makanga pamoja na ukarabati wa shule ya msingi Makanga na uchimbaji wa visima katika kijiji cha mdindo.
Chanzo; Nipashe