Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema uuzwaji wa vileo pamoja na vinywaji vyenye sukari nyingi kwa gharama nafuu katika baadhi ya nchi duniani, unachochea ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza.
WHO imetaja kiwango cha chini cha kodi katika bidhaa hizo kama moja ya sababu ya bidhaa hizo kuuzwa kwa gharama nafuu, jambo linalosababisha kuongezeka kwa magonjwa hayo kama vile kisukari, magonjwa ya moyo, saratani na mengineyo ya aina hiyo.
WHO imeyaeleza hayo katika taarifa yake kwa umma iliyoitoa Januari 13, 2025 baada ya uzinduzi wa ripoti zake mbili za kimataifa, ikitaja makundi ya vijana na watoto kuathirika zaidi na magonjwa hayo.
Katika ripoti hizo WHO imetoa ushauri kwa nchi mbalimbali duniani kuongeza kodi na ushuru katika vinywaji hivyo pamoja na vilevi, jambo ambalo litasaidia kuongeza mapato ya serikali na kupunguza matumizi ya bidhaa hizo.
Imesema fedha iztakazopatikana zitasaidia kuboresha utoaji wa huduma mbalimbali zikiwemo za afya kwa umma.
Chanzo; Mwananchi