Mahenge, eneo lililopo mkoani Morogoro, Wilaya ya Ulanga limeendelea kujipatia umaarufu mkubwa duniani kutokana na madini adimu ya vito aina Spineli, hali ambayo sasa inaliweka eneo hilo katika ramani ya utalii wa madini nchini Tanzania.
Hayo yalibainishwa Novemba 10,2025 na Mhandisi Penina Mtego ambaye ni msimamizi mgodi wa Ruby International unaosimamia uchimbaji wa madini ya Spineli katika kijiji cha Epanko.
Mhandisi Penina alielezea sababu iliyopelekea kuanzishwa kwa kituo cha Utalii wa madini ya Spineli ni kutokana na ubora wa madini hayo ambapo yanapelekea kuonekana kama yanatengenezwa maabara jambo linalopelekea wafanyabiashara wa madini ya vito kimataifa, watafiti na wadau mbalimbali kufika mahenge ili kujionea sehemu halisi yanapochimbwa madini hayo ikiwa pamoja na kutembelea sehemu maalum yanapohifadhiwa.
Mhandisi Penina alifafanua kuwa, madini ya spineli kutoka Mahenge yanajulikana kwa uzuri wake wa kipekee, hususan rangi yake ya waridi na nyekundu inayong’aa, ambayo inavutia wanunuzi na wachimbaji wa vito kutoka mataifa mbalimbali.
Aliongeza kuwa, Spineli ya Mahenge imekuwa ikitajwa mara kwa mara katika maonyesho ya vito ya kimataifa kama Tucson Gem Show nchini Marekani , Hong Kong Jewellery Fair na BangKok Thailand ikiifanya Tanzania kuwa miongoni mwa vyanzo muhimu vya madini bora duniani.
Naye, Salehe Mbura anayesimamia kitengo cha uzalishaji katika mgodi huo alisema kuwa, uwepo wa madini hayo umekuwa chachu ya kuibuka kwa aina mpya ya utalii unaoitwa utalii wa madini, ambapo wageni hutembelea migodi, kujifunza kuhusu malezi ya madini, na kushuhudia shughuli za uchimbaji wa kiasili. Wengine huja kwa ajili ya biashara, utafiti, au kutembelea maeneo ya kihistoria yanayohusiana na uchimbaji wa madini hayo.
Chanzo; Nipashe