Sera mpya ya Fedha inayotumia riba ya Benki Kuu imeanza kuonyesha mafanikio makubwa katika uchumi wa Tanzania, ikiwemo kuongezeka kwa thamani ya shilingi na kudumisha utulivu wa bei.
Meneja Msaidizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), anayeshughulikia Uchumi na Takwimu, Pendaeli Chamicha, alisema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari wa mikoa ya Dodoma, Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Zanzibar kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na Benki Kuu.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Chamicha alisema kuwa sera hii mpya imesaidia kupunguza riba, kudumisha utulivu wa bei na kuimarisha akiba (reserves) za fedha za taifa.
“Kabla ya sera hii, uchumi wa Tanzania ulikabiliwa na changamoto za riba kubwa na bei zisizo thabiti. Lakini sasa tunao uthabiti zaidi katika fedha zetu, na uchumi unaonyesha ukuaji thabiti,” alisema Chamicha.
Aidha, aliongeza kuwa sera ya fedha imesaidia kuweka kipaumbele katika mahitaji makuu ya uchumi, na kurekebisha changamoto zinazojitokeza kwa njia ya “learning by doing”, ambapo BOT inachukua maamuzi ya moja kwa moja kulingana na hali halisi ya uchumi.
Chanzo; Nipashe