Matukio mbalimbali wakati wa ushiriki wa Tanzania katika Jukwaa la 18 la Kimataifa la Chakula na Kilimo (GFFA) yamehusisha mikutano ya uwili ambapo Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo (Mb) amekutana kwa mazungumzo na Waziri wa Kilimo na Usalama wa Chakula wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo, Muhindo Nzangi Butondo.
Viongozi hao wamekutana tarehe 15 Januari 2026, mjini Berlin na kuzungumza kuhusu kuwa na makubaliano ya moja kwa moja ya kibiashara ya nchi hizo mbili katika Sekta ya Kilimo lengo ni kuhakikisha kuwa mazao ya ziada yanayopatikana nchini Tanzania yanauzwa nchini Kongo DRC.
Kufuatia mazungumzo hayo, Waziri Chongolo amekuelekeza Gerald Mweli, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Wataalamu wa Wizara ya Kilimo kuanza na kukamilisha makubaliano hayo ndani ya wiki nne zijazo.
Aidha, katika hatua nyingine Waziri Chongolo amekutana na Rana Tanveer Hussain, Waziri wa Kilimo, Usalama wa Chakula na Utafiti wa Kitaifa wa Pakistan wakati wa ufunguzi rasmi wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula na Kilimo (GFFA), nchini Ujerumani tarehe 15 Januari 2026.
Vilevile Waziri Chongolo amekutana kwa mazungumzo na Dkt. Helmut Fluhrer, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Rain Maker ya nchini Ujerumani tarehe 15 Januari 2026, jijini Berlin.
Viongozi wengine wanaoshiriki katika Jukwaa la GFFA ni Gerald Mweli, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Raymond Mndolwa, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) Gungu Mohamed Mibavu, Mkurugenzi wa Masoko na Usalama wa Chakula Wizara ya Kilimo, Irene Madeje Mlola, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Tagie Daisy M., Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali wa Wizara ya Kilimo, na wataalamu wa diplomasia na kilimo.
Chanzo; Millard Ayo