Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Zanzibar kimemkana mwanachama wake, Said Issa Mohamed, kikisema kuwa kesi aliyofungua Mahakama Kuu si ya chama bali ni hatua yake binafsi.
Said Issa Mohamed kwa kushirikiana na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa CHADEMA kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu, walifungua kesi katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.
Katika kesi hiyo, walifungua madai dhidi ya Bodi ya Wadhamini ya CHADEMA pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, wakidai kuwapo mgawanyo usio sawa wa mali na rasilimali za kifedha za chama kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Wadai hao wanadai hali hiyo inakiuka Sheria ya Vyama vya Siasa pamoja na Katiba ya chama hicho. Aidha, wameeleza pia kuwepo viashiria vya ubaguzi wa kidini na kijinsia pamoja na matamko wanayodai yanaweza kuvuruga Muungano.
Juzi, Said Issa Mohamed aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza kuwa kufungua kesi hiyo ni kwa ajili ya kulinda maslahi ya CHADEMA Zanzibar.
Hata hivyo, jana CHADEMA Zanzibar ilitoa taarifa rasmi iliyosainiwa na Mkuu wa Idara ya Habari na Uenezi, Hamad Mussa Yusuf, ikikanusha madai hayo na kutoa hoja kadhaa za kumtenga na hatua aliyoichukua.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kesi hiyo si ya CHADEMA Zanzibar bali ni ya Said Issa Mohamed pamoja na watu au makundi yanayodaiwa kumshawishi au kumtuma kufungua shauri hilo.
Chanzo; Nipashe