Mwenyekiti Mstaafu wa CHADEMA, Freeman Mbowe amesema haamini kama kuna kiongozi yeyote wa CHADEMA anaweza kutoka hadharani na kusema kuwa Chama hicho kimetengwa katika kushiriki katika msiba wa Muasisi wa Chama hicho Mze Edwin Mtei ambapo amesema kuwa taarifa za mtandaoni zipuuzwe na hazina ukweli wowote.
Mbowe ameyasema hayo hii leo wakati akijibu Swali la mwandishi wa habari wa Ayo Tv, kuhusu kusambaa kwa taarifa mtandaoni zinazoeleza ya kuwa CHADEMA imetengwa na kupewa muda wa asubuhi wa kutoa salamu za rambirambi ambapo amesema kuwa taarifa hizo sio za kweli na hakuna aliyetengwa.
“Taarifa za mitandao zipo na kila siku zipo na kwamba zina ukweli kiasi gani hilo ni jambo lingine na nyinyi ni Waandishi wa Habari mnajua media yeyote ina utaratibu wa kuthibitisha habari zake sasa kwenye mitandao ya kijamii mtu yeyote anaweza kuamua kurusha atakacho amua kurusha lakini nyie mmekuwa hapa wakati wote Watu asilimia karibia 80 wote hapa ni viongozi wa CHADEMA, wanatengwaje? Wakati wameshirikishwa katika kila hatua, hakuna mtu yoyote aliyetengwa na hakuna ataye tengwa.” Amesema Freeman Mbowe.
Chanzo; Millard Ayo