ukio la kusikitisha limeripotiwa nchini Thailand baada ya mwanaume mwenye umri wa miaka 44 kufariki dunia akidaiwa kuishi kwa karibu mwezi mmoja akinywa pombe pekee bila kula chakula.
Kwa mujibu wa taarifa za eneo hilo, mwanaume huyo alikuwa akipitia msongo wa mawazo kufuatia talaka hali iliyomfanya kuacha kula chakula cha kawaida na badala yake kunywa bia kila siku.
Afya yake ilizidi kudhoofika taratibu kutokana na kukosa lishe na maji ya kutosha katika kipindi hicho.
Mwili wake uligunduliwa nyumbani kwake katika wilaya ya Ban Chang District, mkoa wa Rayong baada ya mwanae mwenye umri wa miaka 16 kurejea kutoka shuleni na kumkuta baba yake akiwa hajitambui kufuatia kile kilichoonekana kama kifafa.
Kijana huyo alipiga simu kuomba msaada wa dharura lakini wahudumu wa uokoaji walipofika walithibitisha kuwa tayari alikuwa amefariki.
Ndani ya chumba chake cha kulala mamlaka zilikuta zaidi ya chupa 100 za bia zilizo tupu zikiwa zimepangwa sakafuni karibu na kitanda.
Inasemekana chupa hizo zilipangwa kwa namna iliyobaki na njia nyembamba tu ya kupita jambo lililoonyesha kiwango kikubwa cha matumizi ya pombe kabla ya kifo chake.
Maafisa wanaamini kuwa unywaji pombe kupita kiasi pamoja na kukosa chakula huenda vilichangia kwa kiasi kikubwa kifo hicho ingawa uchunguzi wa kitabibu (autopsy) ulitarajiwa kufanyika ili kuthibitisha chanzo halisi cha kifo.
Chanzo; Bongo 5