Kuanzishwa kwa Ada ya Uendelezaji wa Miundombinu ya Bandari (PID), kumepokelewa kwa mitazamo tofauti na Wafanyabiashara mbalimbali ambapo wengi wameiona kama mzigo wa gharama kwa Wafanyabiashara na hata kwa Mlaji wa mwisho.
Katika mahojiano na AyoTV, Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano kwa Umma Mamlaka ya Bandari TPA, Dkt. George Frasha, amesema Wafanyabiashara Nchini hawatakiwi kuwa na wasiwasi kufuatia ongezeko hilo na kusema kodi hiyo inalenga kukusanya fedha za kuboresha miundombinu ya Bandari ili kuongeza ufanisi wa huduma na kuimarisha mazingira ya biashara kwa Wadau wanaotumia Bandari.
Kwa mujibu wa Dkt. Frasha, uwekezaji katika miundombinu ya kisasa ni hatua muhimu katika kuhakikisha Bandari za Tanzania zinakuwa na ushindani mkubwa zaidi katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, hivyo maboresho hayo yatasaidia kupunguza ucheleweshaji wa mizigo na kuongeza ufanisi katika mnyororo mzima wa usafirishaji.
Mmoja wa Wafanyabiashara waliozungumza na AyoTV, Mkurugenzi wa BM CARS na mmoja wa Waagiza magari Leonard Magere, amependekeza kufutwa kabisa kwa tozo hiyo mpya akisisitiza kuwa ujio wake unaweza kuumiza wengi na kupelekea kupanda kwa bei za bidhaa sokoni.
Chanzo; Millard Ayo