Dunia inaingia katika kipindi kipya cha gharama kubwa kwenye vifaa vya kiteknolojia hasa simu janja, kufuatia ongezeko la mahitaji ya chipset za kumbukumbu zinazotumika kuendesha mifumo ya AI kwenye simu janja hizo.
Wachambuzi wa masoko wanaeleza kuwa kuanzia 2026, vifaa vipya vya kidijitali vinaweza kuuzwa kwa bei ya juu kuliko ilivyozoeleka, huku uzalishaji wake ukipungua na mahitaji yakizidi kupanda.
Hii ina maana kwamba watumiaji wanaotegemea kubadilisha simu janja au kompyuta kila mwaka huenda wakalazimika kuchelewa au kulipa zaidi ya ongezeko la kawaida ili kupata kifaa kipya.
Ripoti zinaonyesha kuwa ongezeko hili la gharama halitaathiri tu vipengele vya kifaa, bali pia kasi ya usambazaji wake sokoni. Upatikanaji unaweza kuwa mdogo, bidhaa zikawa adimu, na kampeni za mauzo zikabadilika kutoka "nenda kanunue" hadi "subiri ujipange".
Dunia ikiwa inaendelea kupokea mabadiliko ya teknolojia pamoja na AI kwa ujumla, inahofiwa kupandisha gharama ya vifaa vingi vya kielektroniki mara kwa mwa kadiri mabadiliko ya AI yanavyozidi kukua.
Chanzo; Global Publishers